Kwa kiongozi wa muziki. Zaburi ya Daudi. 1Yahwe, uniokoe dhidi ya waovu; unikinge dhidi ya watu wenye vurugu. 2Wao wanapanga uovu mioyoni mwao; wanasababisha mapigano kila siku. 3Ndimi zao zinajeruhi kama nyoka; sumu ya fira imo midomoni mwao. Selah 4Ee Yahwe, unilinde dhidi ya mikono ya waovu; unikinge na vurugu za watu wanaopanga kuniangusha. 5Wenye majivuno wameweka mtego kwa ajili yangu; wameeneza nyavu; wameweka kitanzi kwa ajili yangu. Selah 6Nilimwambia Yahwe, “Wewe ni Mungu wangu; usikie kilio changu unihurumie.” 7Ee Yahwe, Bwana wangu, wewe ni mwenye nguvu uwezaye kuniokoa; hunifunika ngao kichwa changu siku ya vita. 8Ee Yahwe, usiyatimize matakwa ya waovu; usiruhusu njama zao kufanikiwa. Selah 9Wale wanao nizunguka huinua vichwa vyao; madhara ya midomo yao wenyewe na yawafunike. 10Makaa ya moto na yawaangukie; uwatupe motoni, kwenye shimo refu, wasiweze kuinuka tena. 11Watu wenye ndimi na wasifanywe salama juu ya nchi; na uovu umuwinde kumpiga mtu mwenye vurugu mpaka afe. 12Ninajua kuwa Yahwe atahukumu kwa haki walioteswa, na kuwa atawapa haki wahitaji. 13Hakika watu wenye haki watalishukuru jina lako; watu wanyoofu wataishi uweponi mwako.