Kwa kiongozi wa muziki; kwenye vyombo vya nyuzi. Maschili ya Daudi. 1Uyategee sikio maombi yangu, Mungu; nawe usijifiche mbali na kusihi kwangu. 2Unitazame kwa makini na unijibu; Sina pumziko katika shida zangu 3kwa sababu ya sauti ya adui zangu, kwa sababu ya ukandamizaji wa waovu; maana wananiletea matatizo na kunitesa wakiwa na hasira. 4Moyo wangu wasumbuka ndani yangu, na hofu ya kifo imeniangukia. 5Uwoga na kutetemeka kumenijia, nayo hofu imenielemea. 6Nikasema, “Oh, kama tu ningekuwa na mabawa kama njiwa! Ningelipaa mbali na kupata pumziko. 7Tazama, ningeenda mbali; ningekaa jangwani. Selah 8Ningefanya haraka kuja mafichoni mwako kuzikimbia dhoruba na tufani.” 9Uwaangamize, Bwana, vuruga lugha zao! Kwa maana nimeona vurugu na ugomvi katika mji. 10Mchana na usiku wao huenda kwenye kuta zake; uchafu na ufisadi uko katikati yake. 11Uovu uko katikati yake; ukandamizaji na uongo hauiachi mitaa yake. 12Kwa maana hakuwa adui aliye nikemea, hivyo ningevumilia; wala ingekuwa ni yule aliye nichukia aliyejiinua mwenyewe dhidi yagu, hivyo ningejificha asinione. 13Lakini ulikuwa wewe, mtu sawa na mimi, mwenzangu na rafiki yangu. 14Tulikuwa na ushirika mtamu pamoja; tuliingia katika nyumba ya Mungu tukiwa na umati mkubwa. 15Kifo na kiwapate ghafla; na washuke wakiwa hai kuzimuni, maana ndiko waishiko waovu, hapo hapo kati yao. 16Lakini kwangu mimi, nitamwita Mungu, na Yahwe ataniokoa. 17Wakati wa jioni, asubuhi na mchana ninalalamika na kuomboleza; yeye atasikia sauti yangu. 18Kwa usalama kabisa atayaokoa maisha yangu na vita dhidi yangu, kwa maana wale waliopigana nami walikuwa ni wengi. 19Mungu, yule unayetawala milele, atawasikia na kuwaaibisha wao. Selah Hawabadiliki, na hawamhofu Mungu. 20Rafiki yangu ameinua mikono yake dhidi ya wale waliokuwa na amani naye; Hakuheshimu agano alilokuwa nalo. 21Mdomo wake ulikuwa laini kama siagi, lakini moyo wake ulikuwa adui; maneno yake yalikuwa laini kuliko mafuta, lakini yalikuwa ni panga zilizochomolewa. 22Umtwike mizigo yako Yahwe, naye atakusaidia; yeye hataruhusu mtu mwenye haki kuyumbayumba. 23Bali wewe, Mungu, utawaleta waovu chini kwenye shimo la uharibifu; watu wenye kiu ya kumwaga damu na waongo hawataishi hata nusu ya maisha kama wengine, lakini mimi nitakuamini wewe.