10
Mungu Na Sanamu 
 1 Sikieni lile ambalo Bwana, anena nanyi ee nyumba ya Israeli.  2 Hili ndilo asemalo Bwana: 
“Usijifunze njia za mataifa 
wala usitishwe na ishara katika anga, 
ingawa mataifa yanatishwa nazo. 
 3 Kwa maana desturi za mataifa hazina maana, 
wanakata mti msituni, 
na fundi anauchonga kwa patasi. 
 4 Wanaparemba kwa fedha na dhahabu, 
wanakikaza kwa nyundo na misumari ili kisitikisike. 
 5 Sanamu zao ni kama sanamu 
iliyowekwa shambani la matango kutishia ndege 
nazo haziwezi kuongea; 
sharti zibebwe 
sababu haziwezi kutembea. 
Usiziogope; haziwezi kudhuru, 
wala kutenda lolote jema.” 
 6 Hakuna aliye kama wewe, Ee Bwana; 
wewe ni mkuu, 
jina lako ni lenye nguvu katika uweza. 
 7 Ni nani ambaye haimpasi kukuheshimu wewe, 
Ee Mfalme wa mataifa? 
Hii ni stahili yako. 
Miongoni mwa watu wote wenye hekima 
katika mataifa na katika falme zao zote, 
hakuna aliye kama wewe. 
 8 Wote hawana akili, tena ni wapumbavu, 
wanafundishwa na sanamu za miti zisizofaa lolote. 
 9 Huleta fedha iliyofuliwa kutoka Tarshishi 
na dhahabu kutoka Ufazi. 
Kile ambacho fundi na sonara wametengeneza 
huvikwa mavazi ya rangi ya samawi na urujuani: 
vyote vikiwa vimetengenezwa 
na mafundi stadi. 
 10 Lakini Bwana ni Mungu wa kweli, 
yeye ndiye Mungu aliye hai, Mfalme wa milele. 
Anapokasirika, dunia hutetemeka, 
mataifa hayawezi kustahimili hasira yake. 
 11 “Waambie hivi: ‘Miungu hii, ambayo haikuumba mbingu na dunia, itaangamia kutoka dunia na kutoka chini ya mbingu.’ ” 
 12 Lakini Mungu aliiumba dunia kwa uweza wake, 
akaweka misingi ya ulimwengu kwa hekima yake, 
na akazitandaza mbingu kwa ufahamu wake. 
 13 Atoapo sauti yake, maji yaliyo katika mbingu hunguruma; 
huyafanya mawingu yainuke kutoka miisho ya dunia. 
Hupeleka umeme wa radi pamoja na mvua, 
naye huuleta upepo kutoka ghala zake. 
 14 Kila mmoja ni mjinga na hana maarifa, 
kila sonara ameaibishwa na sanamu zake. 
Vinyago vyake ni vya udanganyifu, 
havina pumzi ndani yavyo. 
 15 Havifai kitu, ni vitu vya kufanyia mzaha tu, 
hukumu yavyo itakapowadia, vitaangamia. 
 16 Yeye aliye Fungu la Yakobo sivyo alivyo, 
kwani ndiye Muumba wa vitu vyote, 
pamoja na Israeli, kabila la urithi wake: 
Bwana Mwenye Nguvu Zote ndilo jina lake. 
Maangamizi Yajayo 
 17 Kusanyeni mali na vitu vyenu mwondoke nchi hii, 
enyi mnaoishi katika hali ya kuzingirwa na jeshi. 
 18 Kwa kuwa hili ndilo asemalo Bwana: 
“Wakati huu, nitawatupa nje kwa nguvu 
wote waishio katika nchi hii; 
nitawataabisha 
ili waweze kutekwa.” 
 19 Ole wangu mimi kwa ajili ya kuumia kwangu! 
Jeraha langu ni kubwa! 
Lakini nilisema, 
“Kweli hii ni adhabu yangu, 
nami sharti niistahimili.” 
 20 Hema langu limeangamizwa; 
kamba zake zote zimekatwa. 
Wana wangu wametekwa na hawapo tena; 
hakuna hata mmoja aliyebaki wa kusimamisha hema langu 
wala wa kusimamisha kibanda changu. 
 21 Wachungaji hawana akili 
wala hawamuulizi Bwana, 
hivyo hawastawi 
na kundi lao lote la kondoo limetawanyika. 
 22 Sikilizeni! Taarifa inakuja: 
ghasia kubwa kutoka nchi ya kaskazini! 
Hii itafanya miji ya Yuda ukiwa, 
makao ya mbweha. 
Maombi Ya Yeremia 
 23 Ninajua, Ee Bwana, kwamba maisha ya mwanadamu si yake mwenyewe; 
hawezi kuziongoza hatua zake mwenyewe. 
 24 Unirudi, Ee Bwana, lakini kwa kipimo cha haki: 
si katika hasira yako, 
usije ukaniangamiza. 
 25 Umwage ghadhabu yako juu ya mataifa 
wasiokujua wewe, 
juu ya mataifa wasioliitia jina lako. 
Kwa kuwa wamemwangamiza Yakobo; 
wamemwangamiza kabisa 
na kuiharibu nchi yake.