1Msifuni Yahwe. Amebarikiwa mtu yule anaye mtii Yahwe, apendezwaye sana na amri zake. 2Kizazi chake kitakuwa ni chenye nguvu duniani; kizazi cha mcha Mungu kitabarikiwa. 3Nyumbani mwake mna utajiri na mali; na haki yake itadumu milele. 4Nuru huangazia gizani kwa ajili ya mtu mcha Mungu; yeye ni wa fadhili, huruma, na haki. 5Heri atendaye fadhili na kukopesha, afanyaye mambo yake kwa uaminifu. 6Kwa maana hataondoshwa kamwe; mwenye haki atakumbukwa milele. 7Haogopi habari mbaya; ni jasiri, akimtumainia Yahwe. 8Moyo wake ni mtulivu, hana woga, mpaka aonapo ushindi dhidi ya watesi wake. 9Huwapa masikini kwa ukarimu; haki yake yadumu milele; atainuliwa kwa heshima. 10Mtu mwovu ataona haya na kukasirika; atasaga meno yake na kuyeyuka; tamaa ya wasio haki itapotea.